Treni ya Japan iendayo kasi imevunja rekodi yake duniani kwa kufikia mwendo wa kilomita 603 kwa saa, sawa na maili 374 kwa saa katika majaribio yake karibu na Mlima Fuji.
Treni hiyo imevunja rekodi yake ya mwendo wa kilomita 590 kwa saa iliyoweka wiki iliyopita katika jaribio lingine.
Treni ya maglev ambayo haitegemei kugusana na chuma bali inaendeshwa kwa nguvu ya umeme, inatumia sumaku zilizochajiwa kwa umeme kunyanyua na kuvuta mabehewa juu ya njia ya reli.
Treni ya Kati ya Japan, JR Central, ambayo inamiliki matreni hayo, inataka kuanzisha huduma yake kati ya Tokyo na mji wa Nagoya uliopo katikati ya Japan, ifikapo mwaka 2027.
Safari hiyo ya kilomita 280 itachukua dakika itachukua muda wa dakika 40 tu, pungufu ya nusu ya muda unaotumiwa sasa.
Hata hivyo abiria hawatashuhudia treni hiyo kukimbia mwendo wake uliovunja rekodi kwa sababu kampuni inasema treni zake zitakimbia kasi ya kilomita 505 kwa saa. Kwa kulinganisha treni za mwendo kasi kabisa za Japan aina ya shinkansen, au "bullet train" inakimbia mwendo kasi wa kilomita 320 kwa saa.
Majaribio ya treni hiyo yalifanyika katika reli ya majaribio katika mkoa wa Yamanashi ulioko katikati mwa Japan.
Ujenzi wake unakadiriwa kugharimu karibu dola za kimartekani bilioni 100 au pauni za Uingereza bilioni 67 kwa ujenzi tu wa kwenda Nagoya, ambapo asilimia 80% ya gharama itakwenda katika ujenzi wa mahandaki ya kupitia treni hiyo.
Ifikapo mwaka 2045, treni hizo za mwendo kasi za maglev zinatarajiwa kusafiri kati ya miji ya Tokyo na Osaka kwa muda wa saa moja tu na kupunguza urefu wa safari kwa nusu ya muda uliokuwa ukitumika yaani saa mbili.
Watu wapatao 200 walijipanga kando ya reli kushuhudia majaribio ya treni hiyo yaliyofanyika Jumanne.
"Jinsi treni inavyokwenda kwa mwendo kazi zaidi, ndivyo inavyozidi kutulia- nafikiri ubora wa treni umeimarika," amesema mkuu wa utafiti wa treni ya JR Central, Yasukazu Endo.
 
Top